Jumatatu 3 Agosti 2026 - 06:45
Ulaya na Israel hawana uwezo wa kuidhibiti Yemen

Hawza/ Kamanda wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la utawala wa Kizayuni, akikiri kushindwa kwa Israel na nchi za Ulaya katika kukabiliana na Yemen, amesisitiza kuwa; uwezo wa kuzuia (deterrence) ulioundwa na Yemen katika Bahari Nyekundu haujavunjwa, na hadi sasa hakuna suluhisho madhubuti lililopatikana la kuudhibiti.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu YDH, Eliezer Marom, Kamanda wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la utawala wa Kizayuni na mtafiti mwandamizi katika Kituo cha Tafiti za Kimkakati cha Begin–Sadat, katika mahojiano na gazeti la Maariv, alisema kuwa; mkutano kati ya Benjamin Netanyahu na Donald Trump haukuwa na mafanikio yoyote ya kivitendo. Alisema mkutano huo uliandaliwa zaidi kwa malengo ya kisiasa na ya kipropaganda kuliko kuleta matokeo yoyote yanayoonekana.

Akieleza kuwa uwezo wa Yemen wa kuzuia shughuli za kijeshi katika Bahari Nyekundu sasa umegeuka kuwa "uhalisia unaokubalika" katika duru za kijeshi za Israel, alisema: Mkutano huo ulifanyika kwa lengo la kutuma ujumbe wa kisiasa tu, na haukuwa ishara ya mafanikio yoyote muhimu ya kidiplomasia.

Marom, akiukosoa namna mkutano huo ulivyoendeshwa, alisema: "Kama kungekuwa na jambo muhimu na la siri, pande hizo mbili zingezungumza kwa faragha. Lakini wajumbe wote wa pande zote walikuwepo, misimamo inayojulikana ya Israel ilirudiwa, wakapeana mikono, wakatabasamu, na kikao kikaisha. Kwa mikutano ya aina hii haiwezekani kufanikisha jambo kubwa."

Pia alisema kuwa; mkutano huo uliathiriwa na maslahi ya uchaguzi wa kisiasa wa pande zote mbili, akieleza kwamba wanasiasa hao wawili wanahitaji picha na mikutano ya aina hiyo kwa ajili ya maonesho ya vyombo vya habari.

Yemen imeweka mizania mpya katika biashara ya baharini

Kamanda huyo wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la utawala wa Kizayuni, akiendelea kuzungumzia maendeleo katika Bahari Nyekundu, Mlango wa Bab al-Mandab na Mlango wa Hormuz, alisema kuwa; kuruhusiwa kwa meli za kubeba mafuta za China kupita Bab al-Mandab ni matokeo ya kuundwa kwa mlingano mpya kati ya China, Iran na Yemen.

Kwa mujibu wake, hali hiyo ni mwendelezo wa ushindani wa kimkakati kati ya Marekani na China, na ni jambo lisilo na manufaa kwa Washington.

Marom pia alikiri kuwa Bandari ya Eilat kwa muda mrefu imekuwa nje ya mzunguko wa shughuli zake za kawaida, lakini akasema suala hilo halijapata mwitiko unaostahili katika kiwango cha kimataifa. Aidha, alidai kuwa biashara ya dunia imejirekebisha kwa kutumia njia mbadala kupitia kusini mwa Afrika, na kwamba kuongezeka kwa muda wa usafirishaji hadi sasa hakujasababisha athari kubwa katika bei za bidhaa.

Ulaya haina uwezo wa kukabiliana na Yemen

Marom, akizungumzia udhaifu wa uwezo wa majeshi ya wanamaji ya nchi za Ulaya, alisisitiza kuwa; meli za kivita za Ulaya, hususan za Uingereza, hazina tena uwezo wa kukabiliana na vitisho vinavyotokana na Yemen, na nyingi kati yake kimsingi hazina uwezo wa kujibu hali hiyo.

Alidai kuwa hali hiyo ni matokeo ya miaka mingi ya kupunguzwa kwa uwekezaji wa nchi za Ulaya katika sekta ya ulinzi, na kwamba nchi hizo zilitumia rasilimali zao katika ustawi wa jamii badala ya kuimarisha uwezo wao wa kijeshi.

Kwa mujibu wa Marom, nchi pekee yenye uwezo wa kufanya uvamizi wa kijeshi wenye ufanisi dhidi ya Yemen ni Marekani, na kwamba Israel inapaswa kuratibu hatua zake na Washington katika suala hilo.

Hakuna suluhisho kwa suala la Yemen

Kamanda huyo wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la utawala wa Kizayuni pia alieleza kuwa kutegemea makundi yenye silaha ya kusini mwa Yemen ili kukabiliana na serikali ya Sana'a si jambo la uhalisia. Alikumbusha kuwa Saudi Arabia na Falme za Kiarabu (UAE) hapo awali pia zilitegemea makundi hayo, lakini hazikuweza kufikia malengo yao.

Akizungumzia msukumo wa kiitikadi wa vikosi vya Yemen, alisema kuwa; kuvishinda au kuvinyima uwezo wao wa kijeshi ni jambo gumu sana.

Mwishoni, Marom akikumbushia kwamba hata Marekani iliwahi kusitisha mashambulizi yake na kufikia makubaliano na Yemen. Alisisitiza: "Katika hali ya sasa hakuna suluhisho maalumu kwa suala hili." Akaongeza kuwa; Yemen sasa imekuwa ni uhalisia wa kiutendaji unaodhibiti eneo lake pamoja na bandari zake, jambo ambalo kwa mujibu wake hadi sasa halijapatiwa suluhisho la mwisho.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha